Tuesday, 30 December 2014

R.I.P WASANII WETU! KINACHOWAUA KWA KASI CHAJULIKANA

MWAKA 2014 unakatika, matukio ya kukumbukwa ni pamoja na wasanii Bongo kupoteza maisha katika mazingira yasiyotarajiwa, Ijumaa linakupa hatua kwa hatua.Kumbukumbu za haraka zinabainisha kuwa, tangu mwaka 2011 mpaka 2014, wasanii  wenye majina makubwa na madogo wasiopungua 32 wamefariki dunia kwa sababu mbalimbali.

Inauma sana! Katika kipindi cha miaka mitatu kuwapoteza wasanii kwa kiasi hicho ni pigo kubwa kwa tasnia, hasa filamu na muziki, ukiwemo wa muziki wa Injili.
Leo katika toleo hili maalum, Ijumaa linawakumbusha wasanii hao walioaga dunia na namna vifo vyao vilivyotokea.

ALBERT MANGWEHA ‘NGEA’
Alikuwa msanii wa Bongo Fleva. Akiwa na miaka 31 alifariki dunia Mei 28, 2013 nchini Afrika Kusini. Chanzo cha kifo chake inadaiwa ni matumizi yaliyopitiliza  ya madawa ya kulevya. Alizikwa Morogoro, Tanzania, Juni 6, 2013.
LANGA KILEO ‘RAIS WA GHETO’
Alikuwa msanii wa Bongo Fleva. Alifariki dunia Juni 13, 2013 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar akiwa na miaka 28. Kifo chake kilithibitishwa kuwa, kilitokana na kuzidiwa na Ugonjwa wa Malaria. Alizikwa  Juni 17, kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar.
MUHIDIN GURUMO ‘MAALIM’
Alikuwa mkongwe wa muziki wa dansi Bongo. Mpaka kifo chake kilichotokea Aprili 13, mwaka huu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili akiwa na miaka 74, alikuwa mwanamuziki wa Msondo Music Band. Kifo chake kilisababishwa na kusumbuliwa na matatizo ya moyo. Alizikwa Aprili 15 kwenye Makaburi ya Kijiji cha Masaki, Kisarawe, Pwani.
FATUMA BINTI BARAKA ‘BI KIDUDE’
Alikuwa mwanamuziki wa taarab. Alifariki dunia Aprili 17 2013 Bububu mjini Zanzibar akiwa na miaka inayodaiwa haipungui mia moja. Alizikwa siku iliyofuata, kwenye Makaburi ya Bububu, Zanzibar.
SHEM IBRAHIM KALENGA
Alikuwa mwanamuziki wa dansi. Alifariki dunia Desemba 15, mwaka huu kwenye Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam akiwa na miaka 64. Haijathibitishwa ugonjwa uliomuua. Alizikwa Desemba 16 kwenye Makaburi ya Kisutu, Dar.
MWANAISHA MOHAMED MBEGU ‘AISHA MADINDA’
Alitikisa kwenye eneo la unenguaji kwenye bendi ya muziki wa dansi. Alifariki dunia Desemba 17, mwaka huu Mwananyamala, Dar es Salaam akidaiwa kuchomwa sindano yenye madawa ya kulevya kiasi cha kuwa sumu kali mwilini. Alizikwa Desemba 19 kwenye Makaburi ya Kigamboni jijini Dar. Mpaka kifo chake alikuwa na miaka 35.
SUDI MOHAMED ‘MCD’
Alikuwa mpiga tumba kwenye Bendi ya The Afrcan Stars ‘Twanga Pepeta’. Alifariki dunia Januari 27, mwaka huu mjini Moshi akisumbuliwa na matatizo ya kifua. Alizikwa Januari 28, mwaka huu kwenye Makaburi ya Njoro, Mjini Moshi.
HAMIS KAYUMBU ‘AMIGOLAS’
Alikuwa mwimbaji wa zamani wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’. Alifariki dunia Novemba 9, 2014 kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa siku kadhaa akisumbuliwa na matatizo ya moyo. Alizikwa Novemba 10, kwenye Makaburi ya Kisutu jijini Dar.
STEVEN KANUMBA
Alikuwa msanii nyota wa filamu za Bongo. Alifariki dunia Aprili 7, 2012, Sinza jijini Dar baada ya kuangukia sehemu ya nyuma ya kisogo. Mpaka anaaga dunia, Kanumba alikuwa na miaka 28. Alizikwa Aprili 10, kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar akiwa na miaka 28.
MARIAM KHAMIS ‘PAKA MAPEPE’
Alikuwa mwanamuziki wa taarab wa Bendi ya Tanzania One Theatre ‘TOT’. Alifariki dunia Novemba 13, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar kwa matatizo ya uzazi wakati akijifungua. Alizikwa Novemba 14 kwenye makaburi ya Magomeni, Dar.
GEORGE OTIENO ‘TYSON’
Alikuwa msanii na mwongozaji wa filamu za Bongo. Alifariki dunia Mei 31, mwaka huu kwa ajali ya gari mkoani Morogoro akiwa na miaka 31. Alizikwa Juni 14, Kijiji cha Siaya, Kenya.
AMINA NGALUMA ‘JAPANESE’
Anaitwa Amina Ngaluma. Alikuwa mwimbaji wa bendi mbalimbali nchini ikiwamo Double M Sound na African Revolution. Alifariki dunia Mei 15, mwaka huu nchini Thailand baada ya kupatwa na uvimbe kichwani. Alizikwa jijini Dar, Mei 24, 2014 kwenye Makaburi ya Tabata, Dar.
ADAM KUAMBIANA
Alikuwa msanii wa sinema za Bongo. Alifariki dunia Mei 17, mwaka huu, Sinza jijini Dar baada ya kuugua ghafla. Alizikwa Mei 20, kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar akiwa na miaka 38.
RECHO HAULE
Alikuwa msanii wa filamu Bongo. Alifariki dunia Mei 27, mwaka huu kwenye Hospitali ya Lugalo jijini Dar kwa matatizo ya uzazi wakati wa kujifungua akiwa na miaka 26. Alizikwa Mei 30 kwenye Makaburi ya Kisutu, Dar.
ZUHURA MAFTAH ‘MELISA’
Zuhura Maftah ‘Melisa’ (39) alikuwa chipukizi wa Bongo Muvi. Alifariki dunia Septemba 8, 2013 katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar baada ya kusumbuliwa na uvimbe kichwani. Alizikwa kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar.
MZEE MANENTO
Mzee Manento (73) alikuwa msanii wa Bongo Movies. Alifariki dunia Oktoba 29, 2014 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni, Dar baada ya kusumbuliwa na maradhi ya moyo kwa muda mrefu. Alizikwa kijijini kwake, Mamba-Miamba wilayani Same, Kilimanjaro.
JUMA KILOWOKO ‘SAJUKI’
Sajuki (26) alikuwa staa mkubwa wa sinema za Kibongo. Alifariki dunia Januari 1, 2013 katika Hospitali ya Muhimbili, Dar baada ya kusumbuliwa na maradhi ya uvimbe na kansa ya ini. Alizikwa kwenye Makaburi ya Kisutu, Dar.
SAID NGAMBA ‘MZEE SMALL’
Mzee Small (59) alikuwa mkongwe wa vichekesho Bongo. Alifariki dunia Juni 8, 2014 katika Hospitali ya Muhimbili, Dar baada ya kusumbuliwa na kiharusi kwa muda mrefu. Alizikwa kwenye makaburi ya Tabata-Segerea, Dar.
YESAYA AMBIKILE ‘YP’
YP (26) alikuwa msanii wa Bongo Fleva kutoka Kundi la TMK Wanaume Family. Alifariki dunia Oktoba 20, 2014 kwenye Hospitali ya Temeke, Dar baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kifua kwa muda mrefu. Alizikwa kwenye makaburi ya Chang’ombe, Dar.
AHMED ALLY UPETE ‘GEEZE MABOVU’
Geeze Mabovu alikuwa msanii wa Bongo Fleva. Alifariki dunia Novemba 12, 2014 baada ya kuumwa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Alizikwa huko Iringa katika makaburi ya Makanyagio.
JOHN STEFANO MAGANGA
Alikuwa mwigizaji wa sinema za Kibongo. Alifariki dunia Novemba 24, 2012 katika Hospitali ya Muhimbili, Dar baada ya kuugua ghafla. Alizikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar.
JAJI KHAMIS ‘KASHI’
Mwigizaji Kashi alifariki dunia Juni 10, 2013 katika Hospitali ya Muhimbili, Dar alikokimbizwa baada ya kuzidiwa ghafla. Alizikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar.
RAMADHAN MKIETY ‘SHARO MILIONEA’
Sharo alikuwa ni staa wa vichekesho na Bongo Fleva. Alifariki dunia Novemba 26, 2012 baada ya kupata ajali mbaya huko Muheza, Tanga. Alizikwa kijijini kwao, Lusanga, Muheza mkoani Tanga.
SHERRY MAGALI
Sherry alikuwa mchekeshaji na mwigizaji wa sinema za Kibongo. Alifariki dunia Oktoba 21, 2014 kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kuugua kifua kwa muda mrefu. Alizikwa kwenye Makaburi ya Mji Mpya, Morogoro.
Wakati huohuo, taarifa zilizotufikia zinasema kuwa, yule mchungaji aliyewahi kutabiri vifo vya wasanii wawili wa filamu na Bongo Fleva ameibuka tena na kutabiri kuwa, jinamizi la vifo vya wasanii bado lipo ambapo amesema:
“Natabiri tena vifo vya wasanii nchini. Kwamba, hadi kufikia Februari mwakani (2015), wasanii wawili watapoteza maisha.
“Lakini ili kukwepa mauti wasimame katika roho wakimwomba sana Mungu na kutoa sadaka bila kusahau kuwasaidia yatima na wazee.”
Naye mtabiri maafuru nchini, Maalim Hassan Hussein Yahya amesema roho ya mauti kwa wasanii ipo inazunguka, itafanya kazi hiyo kufikia Aprili mwakani. 

No comments:

Post a Comment